Na Thandi Winston na Ebrima Sillah
DAKAR, Feb 10 (TerraViva) – Siku ya kwanza ya mikutano na mijadala katika Kongamano la Jamii la Dunia imeandamwa na vurugu za kutafuta kumbi za mikutano.
Chanzo kutoka ndani ya kamati ya maandalizi ya WSF kiliiambia IPS kuwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Cheikh Anta Diop (UCAD) alifuta vyumba vilivyohifadhiwa kwa ajili ya Kongamano katika maeneo ya chuo hicho. Baada ya mijadala vyumba 40 tu vilipatikana kati ya vyumba vya semina 200 ambavyo hapo kabla vilihifadhiwa kwa ajili ya WSF, na kuanza kutumiwa na wanafunzi waliokuwa wakiendesha masomo yao ya darasani kama kawaida katika vyumba vingine.
“Kwa sasa tunajaribu kufunga mahema kwa ajili ya ukumbi, ili tuweze kufanyia semina,” chanzo hicho kilisema.
Kuna karibu mikutano elfu mbili iliyopangwa kufanyika wiki hii. Washiriki wa WSF wanaowasili katika maeneo ya chuo asubuhi hii walikuta vyumba vingi vikiwa na wanafunzi wanaohudhuria masomo yao.
Kikundi cha haki ya ardhi nchini Brazili kilijikusanya chini ya kivuli cha mti kufanya mjadala juu ya upokonyaji wa ardhi ya wananchi katika Brazili na Afrika. Wengine walitoa sauti zao nje ya jengo la utawala la chuo kikuu.
Mmoja wa waandamanaji, Chilean Carolos Morales, alisema, “Pengine mtu katika chuo hakupenda kongamano kwasababu hata wanafunzi wao wangepata masuala mengi mno kuhusu ubepari wa kisasa na jinsi gani wanapoteza rasilimali za nchi kutokana na uroho.”
Makundi yaliyokuwa yakifanya mijadala na uwasilishaji wa mada yalikuwa yakitafuta kumbi mbadala siku nzima, halafu yalijaribu jinsi yanavyoweza kuhabarisha watu juu ya wapi mikutano inafanyikia. Mikutano mingi ambayo hapo awali ilipangwa kufanyika leo imefutwa.
(END/2011)















